Search This Blog

Friday, July 17, 2020

KATIBU MKUU WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA, PROF. RIZIKI SHEMDOE AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA WAZALISHAJI WA SARUJI NCHINI KUJADILI CHANGAMOTO ZA BEI NA UPATIKAJI WAKE.

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe, Leo tarehe 17 Julai, 2020 amekutana na wazalishaji wa Saruji nchini kujadili changamoto ya bei na upatikanaji wake.

Katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Eneo Huru la Uwekezaji kwa Mauzo Nje ya Nchi (EPZA) Ubungo External jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu alisikiliza maelezo ya wazalishaji hao ambao walieleza changamoto mbalimbali zilizopelekea uhaba na kupanda kwa bei ya Saruji Nchini.

Changamoto zilizoelezwa na wazalishaji hao ni pamoja na Mvua kubwa iliyonyesha nchini katika kipindi cha mwezi Machi, Aprili na Mei ambapo iliathiri zaidi uzalishaji na usafirishaji wa Saruji, pili ni mlipuko wa Ugonjwa wa Korona (COVID 19) ambapo asilimia kubwa ya vipuli vya mitambo vinaagizwa kutoka nje ya nchi, tatu ni ujenzi wa miradi mbalimbali ya serikali inayoendelea nchini kama vile barabara za kisasa, ujenzi wa reli ya kisasa ya mwendokasi, bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa mji wa Serikali na Ikulu mpya ya kisasa jijini Dodoma na ujenzi wa nyumba mpya za wakaazi jijini Dodoma.

Katika kikao hicho Prof. Shemdoe amewashukuru wazalishaji wa Saruji kwa kuitikia wito wa Serikali na kujadili hatma ya taifa lao hasa katika kuondoa kero ya kupanda kwa gharama na pia upatikanaji wa Saruji.

Prof. Shemdoe amesema kuwa kikao hiki kimetoa mwongozo mzuri wa muendelezo wa ushirikiano baina ya wawekezaji na Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali kwani kitendo cha wenye Viwanda kuridhia kwa pamoja kuongeza uzalishaji kufikia kiwango kilichokuwa awali pia kutokupandisha bei kitasaidia bei kushuka na Saruji kupatikana kwa wingi ndani ya muda mfupi.

Wazalishaji hao wa Saruji wamepongeza hatua hii iliyochukuliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwani imekuwa muhimili wa kuwaweka pamoja kuwasikiliza na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo. Wawekezaji hao wapo tayari kushirikiana na Serikali katika kuboresha uchumi wa Nchi na Maisha ya Watanzania.

 

Katibu Mkuu Prof. Riziki Shemdoe, akisikiliza baadhi ya wajumbe waliohudhuria Kikao cha wazalishaji wa Saruji kujadili changamoto ya upatikanaji wa Saruji katika ukumbi wa EPZA, Ubungo External jijini Dar es salaam.

Baadhi ya Wajumbe walioshiriki kikao cha Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara na wazalishaji wa Saruji kujadili changamoto ya upatikanaji wa Saruji nchini.



Prof. Kitila Mkumbo aanza kazi muda mchache mara baada ya kuapiswa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akimuapisha Profesa Kitila Alexander Mkumbo kuwa Waziri wa Viwanda n...