Search This Blog

Tuesday, October 20, 2020

Kikao cha menejimenti ya wizara kwa ajili ya kupitia sera ya viwanda vidogo na biashara ndogo, ukumbi wa chuo kikuu cha kilimo cha Sokoine (SUA) Morogoro.

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe, leo tarehe 20 Oktoba, 2020 ameiongoza menejimenti ya wizara katika kikao kazi cha kujadili mapitio (Background paper) ya sera ya viwanda vidogo na vya kati ya mwaka 2003.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu ndugu Ludovick Nduhiye, wakuu wa Idara na Vitengo kutoka wizara ya viwanda na biashara, wawakilishi kutoka sekta binafsi (TPSF),  Taasisi mbalimbali za serikali  pamoja na wadau wa maendeleo nchini ambao ni Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT).

Prof. Shemdoe amesema kwamba wizara imedhamiria kutunga sera za kuwawezesha wajasirimali wadogo kuendeleza biashara ambapo katika blue print tozo mbalimbali ziliondolewa kwa lengo la kuboresha mazingira bora ya wafanyabiashara. Hivyo katika sera hii itawezesha wajasiliamali kufanya shughuli zao kwa urahisi pia uhakika wa mitaji na mikopo.

Naye Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Prof. Raphael Chibunda ameipongeza wizara kwa maamuzi ya kuchagua eneo la SUA kwa ajili ya kikao kazi hicho pia amesema shughuli za kilimo zinaenda sawia na uendelezaji wa viwanda ambayo ndio ajenda ya nchi hii, hivyo basi ili viwanda vizalishe bidhaa za kutosha ni lazima malighafi za kilimo ziwe za kutosha kukidhi viwanda vyetu, Prof. Chibunda alisema pia sera hiyo itasaidia wakulima wanaojishughulisha na uzalishaji wa mazao ya kilimo kuwezeshwa katika mitaji na mikopo nafuu kuendeleza shughuli zao.

Mapitio ya sera ya viwanda vidogo na biashara ndogo yaliwasilishwa na mtaalamu mwelekezi ambaye ni Dkt. Josephat Kweka na kupokea maoni ya kuboresha maeneo mbalimbali kutoka kwa menejimenti ya wizara na wadau waliohudhuria kikao kazi hiki.

Katibu Mkuu Prof. Riziki Shemdoe akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya wizara mara baada ya ufunguzi wa kikao kazi cha mapitio ya sera ya Viwanda vidogo na biashara ndogo katika ukumbi wa chuo cha SUA, MOROGORO.

Baadhi ya wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na wadau mbalimbali waliohudhuria kikao kazi cha mapitio ya sera ya Viwanda vidogo na biashara ndogo


Katibu Mkuu Prof. Riziki Shemdoe (Aliyesimama) akizungumza wakati wa kikao kazi cha Menejimenti ya wizara cha mapitio ya sera ya Viwanda vidogo na biashara ndogo,  kushoto kwa Katibu Mkuu ni Naibu Katibu Mkuu Ludovick Nduhiye, na kulia kwa Katibu Mkuu ni Mkuu wa Chuo cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Prof. Raphael Chibunda.

TAARIFA KWA UMMA - TANZIA



SALAMU ZA POLE 


20 Oktoba, 2020 - Dodoma

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa anatoa salamu za pole kwa familia, ndugu jamaa na marafiki kufuatia kifo cha Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Prof. Damian M. Gabagambi aliyefariki dunia leo tarehe 20 Oktoba, 2020 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es salaam.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya msiba wa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Natambua mchango wake mkubwa katika kuendeleza Sekta ya Viwanda na Biashara hapa nchini”.

Mhe. Bashungwa ametoa pole kwa menejimenti na wafanyakazi wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na wadau wote wa viwanda na biashara hapa nchini.

“Bwana ametoa na Bwana ametwaa, Jina la Bwana libarikiwe”                                        

Monday, October 12, 2020

Uzinduzi wa Kiwanda cha kuchakata Pamba cha chama kikuu cha Ushirika (KACU LTD).

Naibu Katibu Katibu Mkuu, Lodovick Nduhiye, tarehe 8 Oktoba, 2020 Ameshiriki uzinduzi wa Kiwanda cha kuchakata pamba cha chama kikuu cha Ushirika (KACU LTD) Kilichopo wilaya ya Kahama.

Katika ufunguzi huo Naibu Katibu Mkuu alipata fursa ya kutoa saamu za wizara kwa kupongeza chama cha ushirika kwa hatua hiyo waliyofikia ya kuwa na Vinu vya kuchambulia pamba (ginnery) ambavyo vitasaidia katika kazi kuchambua pamba na kuongeza uzalishaji.

Aidha ameupongeza uongozi wa Kiwanda kwa juhudi kubwa wanazofanya kwani kwa hatua hiyo waliyofikia watasaidia ajira kwa watanzania wenzetu wa Kahama na mikoa ya jirani.

Naibu Katibu Mkuu Ludovick Nduhiye akitoa salamu za Wizara katika hafla ya ufunguzi wa kiwanda cha kuchakata pamba cha Chama Kikuu cha Ushirika (KACU LTD) kilichopo Wilaya ya Kahama.





Prof. Shemdoe atembelea kiwanda cha Nellkanth Chemical L.t.d kilichopo eneo la Amboni jijini Tanga.

Katibu Mkuu wizara ya viwanda na biashara Prof. Riziki Shemdoe ametoa wito kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini waje katika mkoa wa Tanga kwani yapo maeneo mengi ya kuwekeza katika sekta viwanda.

Wito huo aliutoa jana alipotembelea kiwanda cha Nellkanth Chemical L.t.d kilichopo eneo la Amboni jijini Tanga wakati alipofanya ziara ya siku moja.

Prof. Shemdoe alisema kuwa Tanzania inavutia zaidi katika uwekezaji na maeneo mengi ya uwekezaji yapo na yanatekelezwa kwa ajili yao hivyo kuwataka wawekezaji wanaohitaji waje kuwekeza ili walipe kodi, walete ajira na mambo mengine yanayoendana na uwekezaji.

“Wito wangu kwa wawekezaji wengine waje wawekeze Tanzania, waje wawekeze mkoa wa Tanga kuna maeneo mengi sana na magodauni ambayo yapo kwa sasa na yangeweza kutumika kwa ajili ya viwanda, waje wakijua hapa nchini tuna blue print ambayo inatekelezwa kwa ajili ya wawekezaji ili waje walipe kodi na kuleta ajira kwa wananchi wetu” alisema.

Aidha alizungumzia suala la uzalishaji katika kiwanda hicho na kusema kuwa kiwanda hicho kina maeneo makubwa yanayofaa kuwekeza biashara zaidi ya uzalishaji uliopo wa chokaa kwani wana maeneo mengine zaidi ya ekari 2,500 ambayo wanaweza kulima chumvi ambayo imeshaanza kuonekana.

“Eneo hili zamani lilikuwa halilimiki hapa lakini sasa kuna migodi ambayo inatoa madini ambayo inazalishwa na kuleta faida nchini kwani wanalipakodi na kusaidia wananchi kupata ajira, vilevile kuanzishwa kwa shamba hili kutatufanya sisi kuacha kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi” alibainisha.

Hata hivyo alisema kuwa kiwanda hicho kimefanya kazi kubwa kutokana na uzalishaji wake kwani wameajiri wananchi zaidi ya 2,000 ambao wako kiwandani hapo na wengine takribani 4,000 wako kwenye maeneo mengine ambayo yanamilikiwa na mwekezaji huyo.

Naye Mkurugenzi mzalendo wa kiwanda hicho Rashid Amour (Liemba) alisema kuwa kupitia uzalishaji mkubwa wa kiwanda hicho tayari wameshateka masoko katika nchi mbalimbali za Afrika mashariki na Maziwa makuu ambapo wamekuwa wakipeleka bidhaa zao katika masoko ya ushindani.

“Kwakweli mpaka sasa hivi soko letu kubwa liko Congo, lakini siyo Congo pekeyake bali tumeziteka nchi za Kenya, Burundi, Rwanda na Uganda, kwa sasa hivi bidhaa yetu tunashukuru tumezishika nchi zote za Afrika mashariki maana wao ndiyo wanapambana na sisi” alifafanua Liemba.

“Kama mnavyofahamu biashara ni ushindani na sisi tumeingia kwenye ushindani na nchi hizi, tunaiomba serikali iweze kutusaidia katika ushindani huu na kama itatusaidia nina hakika ushindani huu tutaushinda bila matatizo” aliongeza.

Aidha alieleza kwamba kwa sasa ushindani mkubwa wanaoupata ni kutoka nchi ya Afrika kusini ambako pia alizungumzia hofu yake kuhusu soko hilo kwamba nchi ya Congo imeshaingiliwa na nchi ya China ambayo inatengeneza bidhaa hiyo ya chokaa kupeleka huko.

“Kwa sasa hivi ushindani wetu mkubwa uko South Africa kwa Congo, sasa hivi Congo wameingia wachina, wachina wanajitahidi sana kutengeneza bidhaa kuleta hapa nao ni chokaa kama sisi  na mpaka sasa hivi tunajitahidi kupambana nao” aliongeza.

Hata hivyo alibainisha kwamba kiwanda hicho kinapambana katika soko la chokaa lakini zipo biashara nyingine wanazozalisha kama vile magnissium (MGO) ambavyo vyote vinatumika kusafishia cooper ambapo pia alitoa takwimu ya bidhaa wanazosafirisha kupeleka kwenye masoko nje ya nchi.

“Congo peke yake tunapeleka siyo chini ya tani elfu kumi lakini kipindi cha nyumba tulikuwa tunakwenda mpaka tani elfu ishirini, Kenya na Zambia nako pia tunapeleka tani kumi vilevile kwahiyo ni tani elfu ishirini kwa mwezi” alifafanua.

Katibu Mkuu Prof. Riziki Shemdoe akipokea maelezo ya kiwanda cha Nellkanth Chemical L.t.d alipokitembelea kusikiliza changamoto za kiwanda hicho katika ziara yake ya kutembelea Viwanda Mkoani Tanga.




Prof. Kitila Mkumbo aanza kazi muda mchache mara baada ya kuapiswa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akimuapisha Profesa Kitila Alexander Mkumbo kuwa Waziri wa Viwanda n...