Search This Blog

Thursday, April 1, 2021

Prof. Kitila Mkumbo aanza kazi muda mchache mara baada ya kuapiswa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akimuapisha Profesa Kitila Alexander Mkumbo kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 01 Aprili 2021.





Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe (kulia) akimkaribisha Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof, Kitila Mkumbo (kushoto) baada ya kuwasili ofisini muda mchache baada ya kuapiswa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Waziri wa Wizara hiyo katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 01 Aprili 2021. Katikati ni Naibu wa Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb)



Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe (kuliyesimama) akiwatambulisha wakurugenzi wa Wizara hiyo (waliokaa kulia) kwa Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof, Kitila Mkumbo (kushoto) baada ya kuwasili ofisini muda mchache baada ya kuapiswa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Waziri wa Wizara hiyo katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 01 Aprili 2021. aliyekaa wa pili kushoto ni Naibu wa Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb)



Thursday, December 17, 2020

Waziri wa Viwanda na Biashara afanya kikao na Menejimenti ya wizara, wakuu wa taasisi na wafanyakazi jijini Dodoma.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Geoffrey Mwambe (Mb) amewaagiza Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara kutengeneza taarifa ya mawasilisho ya majukumu watakayoyafanya kwa mwaka huu wa fedha.

Pia ametoa siku saba (7) kwa taasisi hizo kupeleka kwake ukomo wa bajeti na mikakati ya tofauti waliojiwekea kwaajili ya kuendeleza na kuleta mabadiliko katika taasisi hizo.

Waziri Mwambe ametoa maagizo hayo Jijini Dodoma wakati alipokutana na wakuu wa taasisi zilizochini ya Wizara, Wakuu wa idara na wafanyakazi ambapo amesema kila taasisi ihakikishe imeweka mikakati mipya ya kuleta mabadiliko katika sekta ya Viwanda na biashara. 

"Ndani ya siku saba (7) kila taasisi itengeneze taarifa na iwasilishwe kwangu juu ya mikakati mikubwa ya kufanyakazi na kuleta mabadiliko makubwa, kila taasisi ilete mikakati yake kujua imepanga kufanya nini" amesema Mhe. Mwambe.

Ametaka kila kitengo katika Wizara hiyo kujitafakari wanafanyaje kazi na wamejipangaje katika kuleta mabadiliko makubwa katika sekta yao ili kuimarisha sekta ya Viwanda na biashara iweze kulinufaisha taifa. 

Aidha ametaka watumishi hao kuwa wabunifu katika nafasi zao za kazi na kutengeneza kitu cha tofauti katika utumishi wao utakaoleta mabadiliko chanya katika sekta ya Viwanda na biashara hapa nchini.

Pia amezitaka taasisi hizo kutengeneza mifumo mipya ya utafutaji wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ili bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini zipate masoko ya ndani na nje ya nchi.


"Tuanze kutafuta masoko ya bidhaa zetu kuna wajasiliamali wanatengeneza bidhaa lakini hawana masoko hawa tunawakatisha tamaa, lakini akizalisha bidhaa na akapata soko inampa nguvu kuendelea kuzalisha zaidi"

 

"Tuwe wabunifu kuna kiwanda nilikitembelea kinazalisha maziwa lakini vifungashio wanafuata Kenya, namuuliza anasema hapa nchini hakuna, nikapita kiwanda kingine wanatengeneza vifungashio vilevile nae anasema hana soko hapa tunafanya uzembe hatuwauganishi hawa wazalishaji" amesema Mhe Mwambe.

Amesema kwa Sasa kuna masoko makubwa ya nje ya nchi ya bidhaa ambapo zinapatikana hapa nchini tena kwa wingi ni wajibu wa taasisi zinazohusika kuhamasisha wananchi kuzalisha bidhaa hizo na kutafuta masoko hayo.

Ameonya baadhi ya watumishi wa taasisi na Wizara kuwa kikwazo cwa kuchelewesha majibu ya maombi ya wafanyabiashara wanapotaka huduma.

"Unakuta mtumishi wa TBS anashirikiana na mshindani wa muomba vibali huyu kila akileta maombi ya kuthibitishwa anaambiwa hajakidhi viwango kumbe wewe unazunguka upande wa pili unachukua fedha" amesema.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb), amewataka watumishi wa Wizara hiyo na taasisi zake kufanyakazi kwa ushirikiano ili kuleta matokeo chanya katika Wizara hiyo."Nataka mshirikiane muwe wamoja mtekeleze majukumu yenu kwa uadilifu na kuwa kiunganishi imara kati ya wafanyabiashara, wakulima na masoko ya bidhaa zao" amesema Mhe. Kigahe.


Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Geoffrey Mwambe akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo alipokutana nao Jijini Dodoma kuweka mikakati ya pamoja namna ya kuendeleza wizara hiyo na kuleta matokeo chanya.


Naibu Waziri wa Viwanda na biashara Mheshimiwa Exaud Kigahe akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo( hawapo pichani) wakati wa kikao cha Waziri wa Viwanda na biashara Mheshimiwa Geoffrey Mwambe, alipokutana nao Jijini Dodoma kuweka mikakati ya pamoja namna ya kuendeleza wizara hiyo na kuleta matokeo chanya.


Baadhi ya Watumishi mbalimbali wa Wizara ya Viwanda na biashara wakimsikiliza Waziri wa Viwanda na biashara Mheshimiwa Geoffrey Mwambe (hayupo pichani) walipokutana na Waziri wa Wizara hiyo Jijini Dodoma kuweka mikakati ya pamoja namna ya kuendeleza wizara hiyo na kuleta matokeo chanya.


Friday, December 11, 2020

Waziri na Naibu waziri wa Viwanda na Biashara wawasili katika ofisi za wizara Mtumba na kupokelewa na Menejimenti pamoja na watumishi wa wizara.

 

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Geofrey Idelphonce Mwambe (Mb) na Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Silaoneka Kigahe (Mb) leo tarehe 10 Desemba, 2020 wameripoti katika ofisi za wizara zilizopo Mtumba jijini Dodoma na kupokekewa na Menejimenti ya Wizara hiyo ikingozwa na Katibu Mkuu Prof Riziki Shemdoe na Naibu Katibu Mkuu ndugu Ludovick Nduhiye.

Wakizungumza na Menejimenti hiyo baada ya kufika ofisini hapo wote kwa pamoja wameomba ushirikiano mkubwa kutoka kwa Watumishi wote wa wizara huku wakisisitiza weledi na kujituma kwenye kazi kwa kila mmoja ndio siri ya mafanikio.

Akizungumza katika kikao kifupi na watendaji hao, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Mwambe amewataka watumishi wote wa Wizara ya Viwanda kuumpa ushirikiano na kufanya kazi kwa kutumia taaluma zao na kuhaidi kufanya kikao kingine na wafanyakazi wote ili kujua changamoto  mbali mbali zinazowakabili watumishi na kuzifanyia kazi.

"Tunashukuru kwa mapokezi yenu yaliyojaa upendo, tunawaahidi ushirikiano, tutafanya vikao na taasisi zetu zote 15 zilizo chini ya wizara na kuzungumza na Wakurugenzi wakuu wa taasisi na pia wakuu wa Idara na vitengo" Alisema Mhe. Mwambe.

Aidha Mhe. Mwambe aliwataka wakuu wote wa Idara zinazosimamia taasisi hizo kuhakikisha zinaleta tija kwa Taifa letu na watanzania kwa ujumla.

Kwa upande wake Naibu Waziri, Mhe. Exaud Silaoneka Kigahe (Mb) amewaomba watumishi wote wa wizara hiyo kumpa ushirikiano kwa kuwa yeye  ni mwenyeji katika Wizara hiyo na kuwataka watumishi  wawe tayari kuendana na mabadiriko yalitokea na kuahidi kuwa atafanya kazi kwa weredi bila kumuonea mtu wala kuumpendelea mtu.

"Niwaombe tushirikiane kama Timu ili tuweze kufika tunapopataka, kwenye sekta zetu hizi yapo mambo ambayo yaliahidiwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kuomba kura kwa wananchi na yapo kwenye Ilani ya CCM, ni kazi yetu kwenda kuyasimamia na kuyatekeleza kama yalivyoelekezwa" Alisema Mhe. Kigahe.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe amewapongeza Mawaziri kwa kuteuliwa kwao na kuwakaribisha huku akihaidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa viongozi hao katika kuijenga Tanzania ya Viwanda.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Geofrey Idelphonce Mwambe (Mb) pamoja na Naibu waziri Mhe. Exaud Kigahe (Mb) baada ya kupokelewa na Katibu wa wizara Prof. Riziki Shemdoe pamoja na Naibu Katibu Ludovick Nduhiye na watumishi wa wizara.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Geofrey Idelphonce Mwambe (Mb) akisalimiana na wafanyakazi wa wizara mara baada ya kuwasili katika ofisi za wizara zilizoko Mtumba jijini Dodoma.



Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Geofrey Idelphonce Mwambe (Mb) akisaini katika ofisi za wizara Mtumba na kufanya majadiliano na Naibu waziri pamoja na Katibu Mkuu pamoja na Naibu Katibu Mkuu.


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Geofrey Idelphonce Mwambe (Mb) pamoja na Naibu waziri Mhe. Exaud Kigahe (Mb) wakipokea zawadi ya ukaribisho kutoka kwa mtumishi wa wizara Bi. Stella Nswima mara baada ya kufika katika ofisi za wizara Mtumba jijini Dodoma.


Sunday, November 15, 2020

Nchi ya Tanzania yang'ara katika maonesho ya Kitamaduni nchini China.

 Wanafunzi wa Tanzania wanaosomea Jiangxi, wameshiriki Maonesho ya Kitamaduni ya Kimataifa International Cultural Festival (ICF) yaliyofanyika tarehe tarehe 14 Novemba, 2020 nchini China.

Maonesho hayo ambayo hufanyika mara moja kwa mwaka yalifadhiliwa na Chuo Kikuu cha Jiangxi cha masuala ya Fedha na Uchumi (JUFE) ambapo yaliwakutanisha wanafunzi wanaoziwakilisha nchi zao, wafanyabiashara na raia mbalimbali wa nchini China.

Katika maonesho hayo wanafunzi wa Tanzania waliweza kuonesha fursa za uwekezaji na biashara katika bidhaa za Korosho, Utalii, mapishi ya chakula cha asili cha Tanzania na madini ya Tanzanite ambapo banda la Tanzania lilikuwa ni miongoni mwa vivutio kutokana na maandalizi yake ambapo lilihusisha utalii wa Tanzania kwa kuonesha picha za video na vipeperushi vilivyotolewa na ubalozi wa Tanzania nchini China.

Katika maonesho hayo kundi la wanafunzi wanaosomea Uzamili kutoka Tanzania ambao pia ni watumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiongozwa na afisa biashara kutoka wizara ya Viwanda na Biashara ndugu, David Geofrey walishiriki kuandaa banda la Tanzania.

Wanafunzi wa kitanzania wanasoma nchini China katika picha ya pamoja waliposhiriki maonesho ya Kitamaduni ya Kimataifa International Cultural Festival (ICF).


Bango likionesha vivutio mbalimbali vinavyopatikana nchini Tanzania.


Raia wa China wakiwa katika banda la Tanzania kuona vivutio mbalimbali vinavyopatikana nchini Tanzania katika maonesho ya Kitamaduni ya Kimataifa International Cultural Festival (ICF).

Tuesday, October 20, 2020

Kikao cha menejimenti ya wizara kwa ajili ya kupitia sera ya viwanda vidogo na biashara ndogo, ukumbi wa chuo kikuu cha kilimo cha Sokoine (SUA) Morogoro.

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe, leo tarehe 20 Oktoba, 2020 ameiongoza menejimenti ya wizara katika kikao kazi cha kujadili mapitio (Background paper) ya sera ya viwanda vidogo na vya kati ya mwaka 2003.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu ndugu Ludovick Nduhiye, wakuu wa Idara na Vitengo kutoka wizara ya viwanda na biashara, wawakilishi kutoka sekta binafsi (TPSF),  Taasisi mbalimbali za serikali  pamoja na wadau wa maendeleo nchini ambao ni Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT).

Prof. Shemdoe amesema kwamba wizara imedhamiria kutunga sera za kuwawezesha wajasirimali wadogo kuendeleza biashara ambapo katika blue print tozo mbalimbali ziliondolewa kwa lengo la kuboresha mazingira bora ya wafanyabiashara. Hivyo katika sera hii itawezesha wajasiliamali kufanya shughuli zao kwa urahisi pia uhakika wa mitaji na mikopo.

Naye Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Prof. Raphael Chibunda ameipongeza wizara kwa maamuzi ya kuchagua eneo la SUA kwa ajili ya kikao kazi hicho pia amesema shughuli za kilimo zinaenda sawia na uendelezaji wa viwanda ambayo ndio ajenda ya nchi hii, hivyo basi ili viwanda vizalishe bidhaa za kutosha ni lazima malighafi za kilimo ziwe za kutosha kukidhi viwanda vyetu, Prof. Chibunda alisema pia sera hiyo itasaidia wakulima wanaojishughulisha na uzalishaji wa mazao ya kilimo kuwezeshwa katika mitaji na mikopo nafuu kuendeleza shughuli zao.

Mapitio ya sera ya viwanda vidogo na biashara ndogo yaliwasilishwa na mtaalamu mwelekezi ambaye ni Dkt. Josephat Kweka na kupokea maoni ya kuboresha maeneo mbalimbali kutoka kwa menejimenti ya wizara na wadau waliohudhuria kikao kazi hiki.

Katibu Mkuu Prof. Riziki Shemdoe akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya wizara mara baada ya ufunguzi wa kikao kazi cha mapitio ya sera ya Viwanda vidogo na biashara ndogo katika ukumbi wa chuo cha SUA, MOROGORO.

Baadhi ya wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na wadau mbalimbali waliohudhuria kikao kazi cha mapitio ya sera ya Viwanda vidogo na biashara ndogo


Katibu Mkuu Prof. Riziki Shemdoe (Aliyesimama) akizungumza wakati wa kikao kazi cha Menejimenti ya wizara cha mapitio ya sera ya Viwanda vidogo na biashara ndogo,  kushoto kwa Katibu Mkuu ni Naibu Katibu Mkuu Ludovick Nduhiye, na kulia kwa Katibu Mkuu ni Mkuu wa Chuo cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Prof. Raphael Chibunda.

TAARIFA KWA UMMA - TANZIA



SALAMU ZA POLE 


20 Oktoba, 2020 - Dodoma

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa anatoa salamu za pole kwa familia, ndugu jamaa na marafiki kufuatia kifo cha Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Prof. Damian M. Gabagambi aliyefariki dunia leo tarehe 20 Oktoba, 2020 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es salaam.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya msiba wa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Natambua mchango wake mkubwa katika kuendeleza Sekta ya Viwanda na Biashara hapa nchini”.

Mhe. Bashungwa ametoa pole kwa menejimenti na wafanyakazi wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na wadau wote wa viwanda na biashara hapa nchini.

“Bwana ametoa na Bwana ametwaa, Jina la Bwana libarikiwe”                                        

Monday, October 12, 2020

Uzinduzi wa Kiwanda cha kuchakata Pamba cha chama kikuu cha Ushirika (KACU LTD).

Naibu Katibu Katibu Mkuu, Lodovick Nduhiye, tarehe 8 Oktoba, 2020 Ameshiriki uzinduzi wa Kiwanda cha kuchakata pamba cha chama kikuu cha Ushirika (KACU LTD) Kilichopo wilaya ya Kahama.

Katika ufunguzi huo Naibu Katibu Mkuu alipata fursa ya kutoa saamu za wizara kwa kupongeza chama cha ushirika kwa hatua hiyo waliyofikia ya kuwa na Vinu vya kuchambulia pamba (ginnery) ambavyo vitasaidia katika kazi kuchambua pamba na kuongeza uzalishaji.

Aidha ameupongeza uongozi wa Kiwanda kwa juhudi kubwa wanazofanya kwani kwa hatua hiyo waliyofikia watasaidia ajira kwa watanzania wenzetu wa Kahama na mikoa ya jirani.

Naibu Katibu Mkuu Ludovick Nduhiye akitoa salamu za Wizara katika hafla ya ufunguzi wa kiwanda cha kuchakata pamba cha Chama Kikuu cha Ushirika (KACU LTD) kilichopo Wilaya ya Kahama.





Prof. Shemdoe atembelea kiwanda cha Nellkanth Chemical L.t.d kilichopo eneo la Amboni jijini Tanga.

Katibu Mkuu wizara ya viwanda na biashara Prof. Riziki Shemdoe ametoa wito kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini waje katika mkoa wa Tanga kwani yapo maeneo mengi ya kuwekeza katika sekta viwanda.

Wito huo aliutoa jana alipotembelea kiwanda cha Nellkanth Chemical L.t.d kilichopo eneo la Amboni jijini Tanga wakati alipofanya ziara ya siku moja.

Prof. Shemdoe alisema kuwa Tanzania inavutia zaidi katika uwekezaji na maeneo mengi ya uwekezaji yapo na yanatekelezwa kwa ajili yao hivyo kuwataka wawekezaji wanaohitaji waje kuwekeza ili walipe kodi, walete ajira na mambo mengine yanayoendana na uwekezaji.

“Wito wangu kwa wawekezaji wengine waje wawekeze Tanzania, waje wawekeze mkoa wa Tanga kuna maeneo mengi sana na magodauni ambayo yapo kwa sasa na yangeweza kutumika kwa ajili ya viwanda, waje wakijua hapa nchini tuna blue print ambayo inatekelezwa kwa ajili ya wawekezaji ili waje walipe kodi na kuleta ajira kwa wananchi wetu” alisema.

Aidha alizungumzia suala la uzalishaji katika kiwanda hicho na kusema kuwa kiwanda hicho kina maeneo makubwa yanayofaa kuwekeza biashara zaidi ya uzalishaji uliopo wa chokaa kwani wana maeneo mengine zaidi ya ekari 2,500 ambayo wanaweza kulima chumvi ambayo imeshaanza kuonekana.

“Eneo hili zamani lilikuwa halilimiki hapa lakini sasa kuna migodi ambayo inatoa madini ambayo inazalishwa na kuleta faida nchini kwani wanalipakodi na kusaidia wananchi kupata ajira, vilevile kuanzishwa kwa shamba hili kutatufanya sisi kuacha kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi” alibainisha.

Hata hivyo alisema kuwa kiwanda hicho kimefanya kazi kubwa kutokana na uzalishaji wake kwani wameajiri wananchi zaidi ya 2,000 ambao wako kiwandani hapo na wengine takribani 4,000 wako kwenye maeneo mengine ambayo yanamilikiwa na mwekezaji huyo.

Naye Mkurugenzi mzalendo wa kiwanda hicho Rashid Amour (Liemba) alisema kuwa kupitia uzalishaji mkubwa wa kiwanda hicho tayari wameshateka masoko katika nchi mbalimbali za Afrika mashariki na Maziwa makuu ambapo wamekuwa wakipeleka bidhaa zao katika masoko ya ushindani.

“Kwakweli mpaka sasa hivi soko letu kubwa liko Congo, lakini siyo Congo pekeyake bali tumeziteka nchi za Kenya, Burundi, Rwanda na Uganda, kwa sasa hivi bidhaa yetu tunashukuru tumezishika nchi zote za Afrika mashariki maana wao ndiyo wanapambana na sisi” alifafanua Liemba.

“Kama mnavyofahamu biashara ni ushindani na sisi tumeingia kwenye ushindani na nchi hizi, tunaiomba serikali iweze kutusaidia katika ushindani huu na kama itatusaidia nina hakika ushindani huu tutaushinda bila matatizo” aliongeza.

Aidha alieleza kwamba kwa sasa ushindani mkubwa wanaoupata ni kutoka nchi ya Afrika kusini ambako pia alizungumzia hofu yake kuhusu soko hilo kwamba nchi ya Congo imeshaingiliwa na nchi ya China ambayo inatengeneza bidhaa hiyo ya chokaa kupeleka huko.

“Kwa sasa hivi ushindani wetu mkubwa uko South Africa kwa Congo, sasa hivi Congo wameingia wachina, wachina wanajitahidi sana kutengeneza bidhaa kuleta hapa nao ni chokaa kama sisi  na mpaka sasa hivi tunajitahidi kupambana nao” aliongeza.

Hata hivyo alibainisha kwamba kiwanda hicho kinapambana katika soko la chokaa lakini zipo biashara nyingine wanazozalisha kama vile magnissium (MGO) ambavyo vyote vinatumika kusafishia cooper ambapo pia alitoa takwimu ya bidhaa wanazosafirisha kupeleka kwenye masoko nje ya nchi.

“Congo peke yake tunapeleka siyo chini ya tani elfu kumi lakini kipindi cha nyumba tulikuwa tunakwenda mpaka tani elfu ishirini, Kenya na Zambia nako pia tunapeleka tani kumi vilevile kwahiyo ni tani elfu ishirini kwa mwezi” alifafanua.

Katibu Mkuu Prof. Riziki Shemdoe akipokea maelezo ya kiwanda cha Nellkanth Chemical L.t.d alipokitembelea kusikiliza changamoto za kiwanda hicho katika ziara yake ya kutembelea Viwanda Mkoani Tanga.




Wednesday, September 30, 2020

Mafunzo ya wadau kuhusu maadili ya utumishi wa umma na mapambano dhidi ya Rushwa.

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu ndugu  Issa Ng'imba afungua mafunzo ya wadau kuhusu maadili ya utumishi wa umma na mapambano dhidi ya rushwa kazini yaliyofanyika leo tarehe 30 Septemba, 2020 katika ukumbi wa Makao makuu ya jeshi la zima moto na Uokoaji, Dodoma. 

Lengo la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo watumishi wa umma kufanya kazi kwa weledi na kupinga rushwa mahala pa kazi katika kuwahudumia wananchi.

Mafunzo hayo ya siku moja yamehudhuriwa na watumishi wa Wizara kutoka idara na Vitengo.

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu ndugu Issa Ng'imba akifungua mafunzo ya wadau kuhusu maadili ya utumishi wa umma na mapambano dhidi ya rushwa kazini leo tarehe 30 Septemba, 2020


Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Viwanda na Biashara walioshiriki mafunzo ya wadau kuhusu maadili ya utumishi wa umma na mapambano dhidi ya rushwa kazini yaliyofanyika katika ukumbi wa Makao makuu ya jeshi la zima moto na Uokoaji, Dodoma.

Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Viwanda na Biashara walioshiriki mafunzo ya wadau kuhusu maadili ya utumishi wa umma na mapambano dhidi ya rushwa kazini yaliyofanyika katika ukumbi wa Makao makuu ya jeshi la zima moto na Uokoaji, Dodoma.

Thursday, September 24, 2020

Mkutano kati ya Menejimenti ya Wizara na ujumbe kutoka Ubalozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania.

 

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Ally Gugu leo tarehe 24 Septemba, 2020 amekutana na ujumbe kutoka Ubalozi wa Afrika ya kusini nchini Tanzania katika ofisi za Wizara zilizopo mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

Akiongea na ugeni huo, ndugu Ally Gugu alisema kuwa Tanzania na Afrika Kusini zimekuwa kwenye ushirikiano wa kibiashara, kiuchumi na kisiasa kwa muda mrefu tangu kipindi cha kudai uhuru. Hivyo ni jambo jema kushirikiana katika kuendeleza biashara kati ya nchi hizo mbili.

Alisema ushirikiano huo umezidi kuimarika kwa uwepo wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo nchi hizi mbili zilikubaliana kuwa na Hati ya Makubaliano (MoU) ya ushirikiano katika Sekta ya Viwanda na Biashara. Lengo la MoU hiyo ni kuimarisha uhusiano wa kibiashara zaidi kwa kuongeza biashara (trade volume) kwa maslahi ya pande zote mbili ukizingatia Afrika ya Kusini ni moja ya nchi iliyokinara katika uwekezaji barani Afrika.

Naye Kaimu balozi wa Afrika ya Kusini, ndugu Sizwe Mayoli amesema kuwa amefurahi kupata fursa ya kujadili masuala ya ushirikiano wa kiuchumi, kibiashara na uwekezaji baina ya Tanzania na Afrika ya Kusini katika kikao hicho.

Aidha, baadhi ya masuala yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na kupata taarifa ya hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Hati ya Makubaliano (MoU) ya Ushirikiano katika Sekta ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. MoU hiyo inatoa fursa ya kuunda Kamati ya Pamoja ya Biashara na Uwekezaji ktika nchi hizi mbili.

Pia kikao hiki kimehitimishwa kwa pande zote mbili kuunda kamati ya pamoja itakayoshirikisha wajumbe kutoka Tanzania na Afrika ya Kusini ili kushirikiana pamoja katika kutekeleza Hati ya makubaliano (MoU) katika sekta ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.


Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Ally Gugu (wa kwanza kushoto) akizungumza wakati wa kikao na Kaimu balozi wa Afrika ya Kusini, ndugu Sizwe Mayoli walipokutana leo tarehe 24 Septemba, 2020 katika ofisi za Wizara zilizopo mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, kushoto ni ndugu Dumo Siyotula katibu wa siasa wa ubalozi wa Afrika ya kusini

Baadhi ya wajumbe kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki walioshiriki kikao hicho.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Ally Gugu (kushoto) akizungumza na Kaimu balozi wa Afrika ya Kusini, ndugu Sizwe Mayoli wakati wa kikao cha kujadili Hati ya Makubaliano (MoU) ya ushirikiano katika Sekta ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.


............................................................................................................................................................

Imetolewa na:

Kitengo cha Habari na Mawasiliano,

Wizara ya Viwanda na Biashara,

24 Septemba, 2020


Thursday, September 3, 2020

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki S. Shemdoe Leo tarehe 3 Septemba, 2020 ameongoza kikao cha Kamati ya Uongozi (Steering Committee) ya Uwezeshaji Biashara.

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki S. Shemdoe Leo tarehe 3 Septemba, 2020 ameongoza kikao cha Kamati ya Uongozi (Steering Committee) ya Uwezeshaji Biashara katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) jijini Dodoma.

Lengo la kikao hiki lilikuwa ni kujadili utekelezaji wa maelekezo ya mkutano wa kwanza wa kamati hiyo uliofanyika tarehe 13 Februari 2020.

Masuala yaliyojadiliwa na kuidhinishwa ni pamoja na hadidu za rejea (ToR) za kamati ya kitaifa ya uwezeshaji biashara, Maeneo ya kundi A, B na C ya mkataba wa uwezeshaji biashara wa Shirika la Biashara la Dunia (WTO TFA) ambayo yatawasilishwa sekretarieti ya WTO kabla ya tarehe 22 Septemba, 2020.

Utekelezaji wa masuala mengine ya biashara nje ya mkataba wa uwezeshaji biashara, utekelezaji wa  mpango mwelekeo (Roadmap) wa miaka mitano (2020/21 - 2024/2025) na mpango kazi (Action Plan) ya mwaka 2020/2021. Aidha, Kamati imetoa maelekezo ya maboresho ya Mfumo wa taarifa za ufanyaji biashara (National Trade Information Module) kabla ya kufanyiwa uzinduzi rasmi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dr. Mwinyi Talib Haji akizungumza wakati wa kikao cha kamati ya uongozi kilichofanyika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) jijini Dodoma.

Katibu Mkuu, Prof. Riziki Shemdoe katika picha ya pamoja na wajumbe walioshiriki kikao cha kamati ya uongozi kilichofanyika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) jijini Dodoma.


Prof. Kitila Mkumbo aanza kazi muda mchache mara baada ya kuapiswa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akimuapisha Profesa Kitila Alexander Mkumbo kuwa Waziri wa Viwanda n...