ZIARA
YA WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA KATIKA KIWANDA CHA KARATASI CHA MUFINDI PAPER
MILLS - IRINGA.
Waziri
wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa amewapa wiki moja wawekezaji wa
kiwanda cha karatasi cha Mufundi Paper Mills kilichopo eneo la Mgololo, kufika
ofisini kwake Mkoani Dodoma kujieleza kuhusu uendeshwaji wa kiwanda hicho.
Akizungumza
katika ziara yake katika kiwanda hicho kilichopo mkoani Iringa, Mhe. Bashungwa
ameshangazwa na jinsi wawekezaji hao walivyoshindwa kukiendeleza kiwanda hicho
ambacho licha ya kuzalisha chini ya kiwango hakina malighafi ya kuzalisha
karatasi nyeupe.
Mhe.
Bashungwa alisema kiwanda hakionyeshi kama kinaendana na dhumuni la kuanzishwa
kwake hapa nchini.
“Hayati
Mwalimu Nyerere na Mhe. Rais John Pombe Magufuli sera zao zinafanana za
kuendeleza viwanda nchini, lakini hapa sioni kama jambo hilo litafanikiwa”
alisema Mhe. Bashungwa.
“Kiwanda hiki kilijengwa kwa gharama ya dola
260 milioni na kilipo binafsishwa kiliuzwa kwa dola 26 milioni kwa wawekezaji
ikiwa ni pungufu ya asilimia 90 ya thamani yake ya awali”.
Mhe.Bashungwa
alisema fedha hizo dola 26 milioni hazikuingia Serikalini, bali alipewa mwekezaji kwa lengo la kufanyia
ukarabati kiwanda ili kiweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
“Hadi
sasa sijui kama hata kodi mnalipa kwa Serikali, natoa wiki moja nataka uje
Dodoma kwa ajili ya kulizungumza suala hili”.
Mhe. Bashungwa aliongeza kusema kuwa kiwanda
hiki kilitengezwa kwa ajili ya kuondoa tatizo la upatikanaji wa karatasi
nchini.
Aliongeza
kuwa masuala ya usalama ya taifa yana sura tofauti tofauti na hata hili pia linaweza
kuwa suala la usalama wa taifa iwapo mataifa mengine yakikataa kutuuzia
karatasi kwa sababu moja au nyingine, itakuwa ni tatizo kubwa.
“Watu
watatushangaa tunashindwa kutengeza hata karatasi kwa ajili ya watoto wetu
waliopo shuleni”.
Kwa
upande wake muwekezaji katika kiwanda hicho alisema kiwanda kinashindwa
kuzalisha karatasi nyeupe kutokana na uhaba wa malighafi zinazozalisha bidhaa
hiyo, hivyo alimuhaidi Mhe. Waziri kuzalisha karatasi hizo watakapopata utatuzi
wa changamoto hiyo.
Kiwanda
hicho kinazalisha takribani tani 52,000 ambazo huuzwa ndani ya nchi na katika
nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
MWISHO
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Viwanda na Biashara,
22 Januari, 2020.















