Search This Blog

Monday, December 30, 2019

Waziri Bashungwa aitisha kikao kufuatilia maelekezo yake kwenye Kiwanda cha Chai cha Kagera

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa leo tarehe 30.12.2019 ameongoza kikao cha ufuatiliaji wa maelekezo aliyoyatoa tarehe 19.12.2019 alipotembelea kiwanda cha Kagera Tea Company Ltd na Mashamba ya wakulima wa chai Mkoani Kagera.


Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Mhandisi Stella Manyanya Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo,  Mkurugenzi wa Kiwanda cha chai Kagera, na wadau wengine muhimu ukiwemo uongozi wa CRDB Bank, wawakilishi kutoka TSHTDA, OTR, TADB, TCB, TRIT. 
Kwenye kikao hicho Mhe. Waziri ameiagiza Bodi ya Chai Tanzania (TBT), TSHTDA, TRIT  kuwatembela wakulima wa chai ili kuwasaidia kulima chai kwa kiwango kizuri na chenye tija. Vilevile ameagiza iundwe kamati maalum itakayoshirikisha taasisi zote muhimu, kwenda kiwandani na kufanya uchambuzi wa uzalishaji wa kiwanda hicho na pia kuwatembelea wakulima wa chai ili kupata ripoti ambayo itawasidia wakulima kunufaika na kilimo. Ameipa kamati hiyo wiki mbili kukamilisha kazi hiyo na kuwasilisha ripoti ofisini kwake.

Pia amesema mwezi wa kwanza atavitembelea viwanda vya Mponde na Lupemba ili kutafuta mstaakabali mzuri wa viwanda viwanda vyote ya chai nchi.




Friday, December 20, 2019

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara afungua mkutano wa mwaka wa TCCIA


Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Mhandisi Stella Martin Manyanya (Mb.) amefungua mkutano Mkuu wa mwaka wa TCCIA leo tarehe 20/12/2019 katika hotel ya four points ya Sheraton (zamani New Africa Hotel) jijini Dar es Salaam. 
Katika hotuba yake Mhe. Manyanya amewataka TCCIA kuwa chemba ya kutoa dira na kuwaongoza wanachama wake kusimama imara katika kujenga uchumi wa Viwanda. Pia amewataka kutekeleza mkakati wao mpya kwa uadilifu unaolenga kuimarisha TCCIA; kuhakikisha mahusiano mazuri na Serikali; na kuimarisha ofisi za Mikoa na Wilaya ziweze kutoka huduma bora zaidi.

Pichani Mhe. Eng. Stella Manyanya (Mb.) NWVB pamoja na viongozi wa TCCIA wakiwemo pia baadhi ya wawakilishi kutoka mashirika ya kimataifa na mabalozi waliohudhuria mkutano Mkuu wa Mwaka wa TCCIA uliofanyika tarehe 20/12/2019 jijini Dar es Salaam.

Waziri Bashungwa atembelea Kiwanda cha Chai Kagera



Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa Viwanda na Biashara akitembea kwenye shamba la chai alipotembelea Kampuni ya Chai ya Kagera iliyopo eneo la Maruku mkoani Kagera tarehe 19.12.2019


Shamba la chai


ZIARA YA WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA KATIKA KIWANDA CHA CHAI CHA KAGERA TEA COMPANY KILICHOPO MARUKU MKOANI KAGERA

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa, amefanya ziara katika kiwanda cha chai cha Kagera Tea Company kilichopo eneo la Maruku mkoani humo.  Kabla ya kuanza ziara hiyo, Mhe. Waziri alikutana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Brigedia Jenerali Marko Gaguti ambapo alipata taarifa fupi kuhusiana na hali ya Viwanda vya chai Mkoani Kagera.
Mhe. Waziri amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Gaguti kwa juhudi anazozifanya katika kuchochea maendeleo ya Viwanda na ukuzaji wa uchumi mkoani Kagera.
Mhe. Waziri Bashungwa alieleza lengo la ziara ni kuwatembelea wakulima wa chai katika mkoa huo na kukutana na mwekezaji wa kiwanda cha Kagera Tea Company kilichopo eneo la Maruku ambacho kimekua kikisuasua katika uzalishaji.
Akiwa kiwandani hapo Mhe. Bashungwa alikutana na wakulima wa chai ambao ndio wazalishaji wakubwa wa malighafi katika kiwanda hicho. Mkulima Philemon Stambuli alieleza kuwa kilimo kimeshuka kwa asilimia 80 na wakulima wamekata tamaa kutokana changamoto mbalimbali zinazosababishwa na kiwanda hicho.
Alizitaja changamoto hizo ni Wakulima kufanya kazi na kiwanda bila mikataba ya kazi, ambapo inapubguza kipato cha mkulima na uhakika wa ajira. Nyingine ni kucheleweshewa malipo na mmiliki wa kiwanda ambaye ni mzawa. Miezi mitatu sasa imepita, wakulima wanadai zaidi ya milioni 40 kinyume na makubaliano ya kulipwa tarehe 15 ya kila mwezi.
Bwana Stambuli ameeleza changamoto nyingine ni kwa muwekezaji wa kiwanda kuchelewa kuchukua chai baada ya kuvunwa hivyo kupelekea chai kupoteza ubora wake.
Naye Ndugu Nyantaba Yahya Hassan, mkulima wa chai ameeleza changamoto ya kukosa ushirikiano kutoka kwa baadhi watendaji wa Serikali Ofisi ya Wilaya kama afisa kilimo pamoja na wakala wa wakulima wadogo wa chai Tanzania pamoja na taasisi nyingine ambazo zinazohusika katika uendelezwaji wa zao la chai.
Kwa upande wake, mmiliki wa kiwanda hicho amekuwa akilalamikia wakulima wasio waaminifu ambapo wanamuibia na kupeleka kilo chini ya makubaliano.
Baada ya kusikiliza kero kutoka kwa wakulima aliitisha kikao kati ya wakulima na msimamizi wa kiwanda cha Kagera Tea Company ili kujadili kwa pamoja changamoto zote na kusikiliza pande zote mbili ili kutoa maamuzi ya pamoja.
Msimamizi wa kiwanda hicho alikiri kutolipa deni la wakuliima ambalo ni zaidi ya milioni 40, malikimbikizo ya mishahara na madeni ya wafanyakazi kiasi cha shilingi milioni 108,
Mhe. Bashungwa alisikitishwa kwa kupuuzwa kwa maagizo yake aliyoyatoa kwa bodi ya chai tarehe 16 Januari, 2019 akiwa naibu waziri wizara ya kilimo kwamba bodi ikae na wakulima pamoja na muwekezaji na kutatua changamoto zote za wakulima lakini hadi amerudi tena kuwatembelea wakulima hao wa chai tarehe 19 Desemba, 2019 bado anakuta changamoto ni zilezile na maagizo ya Serikali hayajafanyiwa kazi.
Mhe. Bashungwa amewahakikishia kuwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, imedhamiria kuinua zao la chai kwa kuhakikisha wakulima wananufaika na kilimo chao, pia kuhakikisha wakulima wanapata stahiki zao na kwa wakati.
Ameendelea kusema kuwa Serikali itahakikisha minada ya chai inafanyika ndani ya nchi ili kuwasaidia wakulima na kupanua soko la ndani.
Aidha, Mhe. Bashungwa alitoa maagizo kwa mwenye kiwanda kulipa madeni ya wakulima na wafanyakazi kabla mwaka huu haujaisha ifikapo tarehe 31 Desemba, 2019. Mhe. Bashungwa aliahidi kurudi tena kiwandani hapo mapema Januari kuhakikisha kama wakulima wamelipwa.
Nao Wakulima wa chai wa Mkoa wa Kagera wamemshukuru Rais Magufuli kwa kumteua Mhe. Bashungwa kama Waziri wa Viwanda na Biashara kwani amekuwa akiwafuatilia mara kwa mara kutatua kero zao.

MWISHO

Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Wizara ya Viwanda na Biashara,
20 Desemba, 2019




Waziri Bashungwa akiweka saini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Brig. Jen. Marko Kaguti (pichani Kulia) kabla ya kuanza ziara yake kwenye Kampuni ya Chai  

Kiwanda cha Chai cha Kagera  

Pichani Mhe. Bashungwa Waziri wa Viwanda na Biashara akizungumza na wakulima na wamiliki wa Kiwanda cha chai cha Kagera alipotembelea eneo hilo tarehe 19.12.2019 










Sunday, December 15, 2019

Mnyororo wa Thamani wa Biashara ya Samaki Mwanza

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa alipata wasaa wa kutembea mitaani na kuingia mwaloni Mwanza kwa mguu kuangalia hali ya biashara hasa ya mnyororo wa thamani wa samaki aina ya sangara na kubadilishana mawazo na wafanyabiashara wadogo wa maeneo hayo na wavuvi. 

"Nimejifunza kwamba hakuna kinachotupwa, hadi uti wa
mgongo wa samaki unatumiwa kusagwa na kuchanganywa na chakula cha kuku. Ni muhimu kuweka mwalo katika hali ya usafi na kusimamia mnyororo wa thamani wa sangara kuhakikisha tunapata maximum value ya kumnufaisha mvuvi, mfanyabiashara na mapato ya Serikali"


Mhe. Bashungwa akiwa kwenye picha na wafanyabiashara ya samaki alipotembea kwa miguu sokoni humo ili kujionea mnyororo wa biashara ya samaki na mapato yanayopatikana  


Thursday, December 12, 2019

Waziri Bashungwa afungua Kongamano la Wafanyabiashara wa Kanda ya Magharibi

Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa Viwanda na Biashara akihutubia wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Biashara Kanda ya Magharibi Mjini Shinyanga leo tarehe 12.12.2019


Mhe. Innocent Bashungwa Waziri wa Viwanda na Biashara amekuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa Kongamano la Biashara na Wakandarasi wa Kanda ya Magharibi. Kongamano hilo lililoandaliwa na Benki ya CRDB limefanyikia katika Ukumbi wa Mikutano wa NSSF Shinyanga, Tarehe 12 Disemba 2019.
Kongamano hilo lililolenga kujadili na kubadilishana mawazo kuhusu bidhaa mbalimbali zinazotolewa na kubuniwa na Benki ya CRDB, limehudhhuriwa pia na viongozi wa mikoa ya kanda hiyo wakiwemo Mhe. Aggrey Mwanri, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Mwandisi Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa Geita na Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga, Mkuu wa Mkoa Kigoma.
Washiriki wa kongamano hilo lililodhaminiwa na Benki ya CRDB kutoka mikoa ya Kanda ya Magharibi (Shinyanga, Tabora, Geita na Kigoma); walibainisha kuwa huduma zinazoendelea kubuniwa na kutolewa na Benki hiyo zimerahisisha upatikanaji wa mitaji na mikopo kwa Wafanyabiashara na Wakandarasi wa mikoa husika.
Akifungua rasmi Kongamano hilo, Mhe. Bashungwa amewasisitiza Wafanyabiasha, Wakandarasi na washiriki wote kuchamngamkia fursa iliyowekwa na Benki ya CRDB ili kukuza biashara zao na kupata faida zaidi. Alisema kwa kufanya hivyo fursa za ajira kwa vijana wa kanda hiyo zitaongezeka na hatimaye pato la Serikali kuongezeka kupitia ulipaji wa kodi.


MWISHO


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Viwanda na Biashara,
12 Desemba, 2019



Mhe. Aggrey Mwanri, Mkuu wa Mkoa wa Tabora akitoa utangulizi kuhusu Kongamano hilo lililoandaliwa na Benki ya CRDB kwa ajili ya Wafanyabiashara na Wahandisi wa Kanda ya Magharibi

Baadhi ya washiriki wa Kongamano hilo lililofanyikia kwenye Ukumbi wa Mikutano wa NSSF Mjini Shinyanga tarehe 12.12.2019

Viongozi wakibadilishana mawazo baada ya Kongamano hhilo kufunguliwa 


Picha ya Pamoja

Wednesday, December 11, 2019

ZIARA YA WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA KATIKA KIWANDA CHA NGUO CHA MWATEX MKOANI MWANZA

Mhe. Bashungwa akiwa na Kiongozi wa Kiwanda cha Mwatex (wa pili kulia) wakati wa ziara yake kiwandani hapo, ambapo ameunda Tume ya Uchunguzi, kuhusu uendeshwaji wa kiwanda.


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa, amefanya ziara katika kiwanda cha Mwatex (2001) LTD kilichopo mkoani Mwanza leo.  Kiwanda hicho ambacho kilibinafsishwa na Serikali na kupewa mwekezaji Amin Radhanin kimeajiri wafanyakazi zaidi ya 600 na kinaendelea na uzalishaji kwa asilimia 60 kutokana na changamoto mbalimbali.

Aidha katika ziara yake Mhe. Bashungwa alizungumza na uongozi wa kiwanda na pia kusikiliza kero za wafanyakazi, ambapo wafanyakazi walipata fursa ya kumueleza Waziri changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Mtumishi wa kiwanda hicho aliyetambulika kwa jina la Thomas Mashauri alieleza kuwa kuna rushwa katika masuala ya ajira, na kueleza kwamba ili uweze kuajiriwa ni lazima utoe hongo ya kiasi cha shilingi elfu hamsini (50,000) ndipo uajiriwe. Aidha aliongeza kusema kuwa wafanyakazi wanalazimishwa kufanya kazi kwa kutumia mashine mbili kwa wakati mmoja pasipo kuangalia jinsi gani mfanyakazi anaumia.

Ndugu Mashauri aliongeza kuwa wasimamizi katika kiwanda hicho hawana kauli nzuri kwa wafanyakazi na pia wamekuwa wakali.

Pia wafanyakazi wa kiwanda cha MWATEX walieleza changamoto ya upatikanaji wa vipuli (spare parts) vya mashine  mbalimbali  katika kiwanda hicho inayopelekea mashine nyingingi kutokufanya kazi na muda mwingi kutumika kwa ajili ya matengenezo.

Baada ya kusikiliza kero za wafanyakazi na kuona utendaji wa kiwanda usioridhisha Mhe. Bashungwa ameagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, TIRDO, Dar Tech, VETA, SIDO, NDC kuunda kamati maalumu ambayo itatembelea kiwanda hiki na kufanya uchambuzi wa uendeshaji wa kiwanda kwa kushirikiana na msimamizi wa kiwanda.

Mhe. Bashungwa ametoa muda kuchunguza mwenendo wa kiwanda hiki hadi kufikia tarehe 1/1/2020 kamati husika iwe imekamilisha kazi na kukabidhi ripoti yake kwa Waziri.

Aidha Mhe. Bashungwa amesema kwamba ripoti husika itasaidia Serikali katika kutatua changamoto zinazokabili kiwanda hiki ili kiendelee kuzalisha kwa asilimia 100 kama ilivyo mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuhakikisha viwanda vyote vilivyobinafsishwa vinafufuliwa, vinafanya kazi na kuongeza uzalishaji kwa asilimia 100, ili kutengeneza mnyororo wa thamani ya mazao.


MWISHO
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Wizara ya Viwanda na Biashara,
11 Desemba, 2019








Tuesday, December 10, 2019

WAZIRI BASHUNGWA AKUTANA NA MAKAMU MWENYEKITI WA CHAMA CHA KIKOMUNISTI CHA VIETNAM

Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa Viwanda na Biashara akisalimiana na Mhe.Pham Minh, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam leo tarehe 10.12.2019 


Mhe. Innocent Bashungwa Waziri wa Viwanda na Biashara leo tarehe 10 Desemba 2019, amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti kutoka Vietnam Mhe. Pham Minh na ujumbe wake kwenye Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yao ambayo yalijikita kwenye misingi na umuhimu wa ushirikiano wa kidugu baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nchi ya Vietnam, Mhe. Bashungwa alitumia fursa hiyo kumshukuru mgeni huyo na Serikali ya Vietnam kwa kununua Korosho ya msimu 2018/2019 zaidi ya asilimia 70 ya mzigo uliokuwepo.

Naye Mhe. Minh, kwa upande wake aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kudumisha mahusiano mazuri hususan kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), ambacho ndio kinachoongoza Serikali nchini.

MWISHO





Viongozi wakiwa kwenye mazungumzo pamoja na wajumbe waliohudhuria wakifuatilia mazungumzo hayo. 

Sunday, December 8, 2019

Mhe. Bashungwa afanya mkutano na Wamiliki na Wasimamizi wa Viwanda cha Samaki Mwanza

Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa Viwanda na Biashara akiongoza majadiliano kwenye kikao chake na Wamiliki na Wasimamizi wa Viwanda vya Samaki Jijini Mwanza 



MKUTANO WA WAMILIKI NA WASIMAMIZI WA VIWANDA VYA SAMAKI KANDA YA ZIWA  

Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa Viwanda na Biashara leo Desemba 8, amekutana na kufanya kikao na wamiliki na wasimamizi wa viwanda vya samaki vilivyopo Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza.
Kikao hicho ambacho pamoja na mambo mengine, kililenga kwenye kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili wenye viwanda na hatimaye kutafuta ufumbuzi wa pamoja na Serikali kiliandaliwa chini ya mwamvuli wa Chama cha Wasindikaji Samaki na Kampuni za Uvuvi za Viwandani yaani kwa Kiingereza, Tanzania Industrial Fishing and Processors Association (TIFPA).  
Baadhi ya changamoto na kero ambazo wadau hao walizibaini kuzuia maendeleo ya viwanda vya samaki nchini ni pamoja na usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi na nyaraka za kuuza nje, marejesho ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) pamoja na ushuru mkubwa.
Mhe. Bashungwa yuko Jijini Mwanza kwa ziara ya kikazi ambapo anatarajia kutembelea viwanda vilivyopo Jijini humo, na kuzungumza na wafanyakazi ili kubaini changamoto zinazokabili viwanda vya ukanda wa Ziwa Victoria, vilivyopo Jijini humo.   

MWISHO
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Viwanda na Biashara,
08 Desemba, 2019





Mhe. Bashungwa akiwa kwenye picha ya pamoja na Wadau wa Viwanda vya Samaki Jijini Mwanza.  


Thursday, December 5, 2019

Mkutano wa Waziri wa Viwanda na Wadau wa sekta ya nyama na ngozi nchini

Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa Viwanda na Biashara akihutubia kwenye mkutano wake na wadau na wamiliki wa Viwanda vya nyama na ngozi nchini, kwenye ukumbi wa JNICC Jijini Dar es Salaam. 


Licha ya Tanzania kushika nafasi ya pili kwa wingi wa mifugo barani Afrika, lakini bado nchi hainufaiki na takwimu hizo kutokana na ubora mdogo wa mazao au bidhaa zitokanazo na mifugo.
Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa Viwanda na Biashara amebainisha hayo leo wakati alipokutana na kufanya kikao na wadau na wamiliki wa viwanda vya nyama na Ngozi nchini Tanzania kwenye Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
“Hadi sasa Tanzania ina ng’ombe zaidi ya milioni 32, mbuzi zaidi ya milioni 20 na kondoo zaidi ya milioni tano. Ili sekta hii iwe na tija kwenye uchumi wetu ni lazima uzalishaji wa bidhaa za ngozi na nyama unapaswa kuongezeka kwenye viwanda vyetu vya ndani” alibainisha kwenye hotuba yake ya ufunguzi.
Ili kukabiliana na hali hii, Mhe. Bashungwa alisema kuwa tayari ameshaanza mazungumzo na nchi ambazo zinaweza kutoa masoko makubwa ya bidhaa hizo, ambapo zitachangia kwa kiasi kikubwa uzalishaji kuongezeka na pia kuongeza pato la taifa. Ajenda ya Serikali ni kuhakikisha viwanda vinajengwa kwa wingi na kuweka mazingira sahihi ya kulinda bidhaa za viwandani na kuhakikisha viwanda hivyo vinazalisha ili hatimaye vilete faida kwa Tanzania na watu wake.
Kwenye mkutano huo, Mhe. Bashungwa aliweka bayana mikakati ya Serikali kulinda bidhaa hizo kama vile kutoza ushuru wa asilimia 80 ya thamani ya ngozi kuisafirisha nje ya nchi, lakini bado viwanda vya ngozi vinazalisha asilimia arobaini tu ya uwezo wa kuzalisha.  
Kwa upande wa wadau hao waliojitokeza kwa wingi, walisisitiza kuwa Serikali iendelee kuweka mazingira wezeshi na kuweka nia ya dhati na kufanya maamuzi ya kufanya biashara. Wazalishaji na wenye viwanda hawatafanikiwa iwapo Serikali haitaweka mkono wake, ikiwemo kutochelewesha maamuzi muhimu.
“Kwetu sisi wadau tunahitaji kuanza kuboresha mifugo yetu, kwasababu nyama nzuri yenye ubora, inatokana na ng’ombe bora. Hata kama Tanzania ina mifugo mingi lakini hatushindani kwenye soko kwasababu ng’ombe wetu sio bora kwenye export” alisema Mzee Crisant Mzindakaya ambaye anamiliki mifugo na kiwanda.
Majadiliano ya wadau na Serikali yametoa mwanga wa nini kifanyike ili sekta hiyo iwe na tija zaidi kwa taifa ikiwemo kuongeza uzalishaji wa viwanda hivyo. Kati ya viwanda vikubwa tisa vilivyopo nchini, viwanda vitano tu ndio vinavyofanya kazi ambapo vinazalisha chini ya asilimia arobaini ya uwezo wao wa kuzalisha.

MWISHO


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Viwanda na Biashara,
05 Desemba, 2019



Mhe. Bashungwa akiendesha mjadala kwenye kikao hicho ambapo wadau pamoja na Serikali waliweza kutoka na mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto zinazokinzana na ukuaji wa sekta hiyo muhimu nchini.



Pichani juu na chini, washiriki wa mkutano huo wakiwemo taasisi mbalimbali za Serikali kama vile Hazina, Brela, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Mambo ya Nje n.k. wakifuatilia mjadala wa mkutano huo.



Prof. Kitila Mkumbo aanza kazi muda mchache mara baada ya kuapiswa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akimuapisha Profesa Kitila Alexander Mkumbo kuwa Waziri wa Viwanda n...