Pia ametoa siku saba (7) kwa taasisi hizo kupeleka kwake ukomo wa
bajeti na mikakati ya tofauti waliojiwekea kwaajili ya kuendeleza na kuleta
mabadiliko katika taasisi hizo.
Waziri Mwambe ametoa maagizo hayo Jijini Dodoma wakati alipokutana na wakuu wa taasisi zilizochini ya Wizara, Wakuu wa idara na wafanyakazi ambapo amesema kila taasisi ihakikishe imeweka mikakati mipya ya kuleta mabadiliko katika sekta ya Viwanda na biashara.
"Ndani ya siku saba (7) kila taasisi itengeneze taarifa na iwasilishwe kwangu juu ya mikakati mikubwa ya kufanyakazi na kuleta mabadiliko makubwa, kila taasisi ilete mikakati yake kujua imepanga kufanya nini" amesema Mhe. Mwambe.
Ametaka kila kitengo katika Wizara hiyo kujitafakari wanafanyaje kazi na wamejipangaje katika kuleta mabadiliko makubwa katika sekta yao ili kuimarisha sekta ya Viwanda na biashara iweze kulinufaisha taifa.
Aidha ametaka watumishi hao kuwa wabunifu katika nafasi zao za kazi na kutengeneza kitu cha tofauti katika utumishi wao utakaoleta mabadiliko chanya katika sekta ya Viwanda na biashara hapa nchini.
Pia amezitaka taasisi hizo kutengeneza mifumo mipya ya utafutaji
wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ili bidhaa zinazotengenezwa hapa
nchini zipate masoko ya ndani na nje ya nchi.
"Tuanze kutafuta masoko ya bidhaa zetu kuna wajasiliamali
wanatengeneza bidhaa lakini hawana masoko hawa tunawakatisha tamaa, lakini
akizalisha bidhaa na akapata soko inampa nguvu kuendelea kuzalisha zaidi"
"Tuwe wabunifu kuna kiwanda nilikitembelea kinazalisha maziwa lakini vifungashio wanafuata Kenya, namuuliza anasema hapa nchini hakuna, nikapita kiwanda kingine wanatengeneza vifungashio vilevile nae anasema hana soko hapa tunafanya uzembe hatuwauganishi hawa wazalishaji" amesema Mhe Mwambe.
Amesema kwa Sasa kuna masoko makubwa ya nje ya nchi ya bidhaa ambapo zinapatikana hapa nchini tena kwa wingi ni wajibu wa taasisi zinazohusika kuhamasisha wananchi kuzalisha bidhaa hizo na kutafuta masoko hayo.
Ameonya baadhi ya watumishi wa taasisi na Wizara kuwa kikwazo cwa kuchelewesha majibu ya maombi ya wafanyabiashara wanapotaka huduma.
"Unakuta mtumishi wa TBS anashirikiana na mshindani wa muomba
vibali huyu kila akileta maombi ya kuthibitishwa anaambiwa hajakidhi viwango
kumbe wewe unazunguka upande wa pili unachukua fedha" amesema.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb), amewataka watumishi wa Wizara hiyo na taasisi zake kufanyakazi kwa ushirikiano ili kuleta matokeo chanya katika Wizara hiyo."Nataka mshirikiane muwe wamoja mtekeleze majukumu yenu kwa uadilifu na kuwa kiunganishi imara kati ya wafanyabiashara, wakulima na masoko ya bidhaa zao" amesema Mhe. Kigahe.


