Search This Blog

Wednesday, January 22, 2020

ZIARA YA WAZIRI BASHUNGWA KIWANDA CHA KARATASI CHA MUFINDI


ZIARA YA WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA KATIKA KIWANDA CHA KARATASI CHA MUFINDI PAPER MILLS - IRINGA.
            Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa amewapa wiki moja wawekezaji wa kiwanda cha karatasi cha Mufundi Paper Mills kilichopo eneo la Mgololo, kufika ofisini kwake Mkoani Dodoma kujieleza kuhusu uendeshwaji wa kiwanda hicho.
            Akizungumza katika ziara yake katika kiwanda hicho kilichopo mkoani Iringa, Mhe. Bashungwa ameshangazwa na jinsi wawekezaji hao walivyoshindwa kukiendeleza kiwanda hicho ambacho licha ya kuzalisha chini ya kiwango hakina malighafi ya kuzalisha karatasi nyeupe.
            Mhe. Bashungwa alisema kiwanda hakionyeshi kama kinaendana na dhumuni la kuanzishwa kwake hapa nchini.
            “Hayati Mwalimu Nyerere na Mhe. Rais John Pombe Magufuli sera zao zinafanana za kuendeleza viwanda nchini, lakini hapa sioni kama jambo hilo litafanikiwa” alisema Mhe. Bashungwa.
“Kiwanda hiki kilijengwa kwa gharama ya dola 260 milioni na kilipo binafsishwa kiliuzwa kwa dola 26 milioni kwa wawekezaji ikiwa ni pungufu ya asilimia 90 ya thamani yake ya awali”.
            Mhe.Bashungwa alisema fedha hizo dola 26 milioni hazikuingia Serikalini, bali  alipewa mwekezaji kwa lengo la kufanyia ukarabati kiwanda ili kiweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
            “Hadi sasa sijui kama hata kodi mnalipa kwa Serikali, natoa wiki moja nataka uje Dodoma kwa ajili ya kulizungumza suala hili”.
Mhe. Bashungwa aliongeza kusema kuwa kiwanda hiki kilitengezwa kwa ajili ya kuondoa tatizo la upatikanaji wa karatasi nchini.
            Aliongeza kuwa masuala ya usalama ya taifa yana sura tofauti tofauti na hata hili pia linaweza kuwa suala la usalama wa taifa iwapo mataifa mengine yakikataa kutuuzia karatasi kwa sababu moja au nyingine, itakuwa ni tatizo kubwa.
            “Watu watatushangaa tunashindwa kutengeza hata karatasi kwa ajili ya watoto wetu waliopo shuleni”.
            Kwa upande wake muwekezaji katika kiwanda hicho alisema kiwanda kinashindwa kuzalisha karatasi nyeupe kutokana na uhaba wa malighafi zinazozalisha bidhaa hiyo, hivyo alimuhaidi Mhe. Waziri kuzalisha karatasi hizo watakapopata utatuzi wa changamoto hiyo.
            Kiwanda hicho kinazalisha takribani tani 52,000 ambazo huuzwa ndani ya nchi na katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

MWISHO

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Viwanda na Biashara,
22 Januari, 2020.

Prof. Kitila Mkumbo aanza kazi muda mchache mara baada ya kuapiswa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akimuapisha Profesa Kitila Alexander Mkumbo kuwa Waziri wa Viwanda n...