Search This Blog

Sunday, January 19, 2020

Ziara ya Naibu waziri Mhandisi Stella Manyanya (Mb) kiwanda kidogo cha kuchakata zabibu

ZIARA YA NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA KATIKA KIWANDA CHA KUCHAKATA ZABIBU CHA WENDECE, PIA KUZINDUA MASHINE YA KUCHAKATA ZABIBU ILIYOBUNIWA NA TEMDO KWA USHIRIKIANO WA SIDO DODOMA.


NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Mhandisi STELLA MANYANYA (Mb), amesema kunahaja ya kuziwezesha kifedha taasisi za utafiti zinazobuni na kutekeleza teknolojia rahisi hapa nchini ili kufikia lengo la kuwa na viwanda na kufikia uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Naibu Waziri Manyanya ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizindua teknolojia mpya ya mashine ya kukamua mchuzi wa zao la zabibu katika kiwanda kidogo Cha WENDECHE kilichopo Kata ya Hombolo Bwawani, iliyobuniwa na TEMDO kwa kushirikiana na SIDO.

Alisema kuna haja ya kuziwezesha taasisi kama SIDO, TEMDO, CAMATEC, TIRDO na nyinginezo, kwani kwa muda mrefu taasisi hizo zilikuwepo lakini hazikuweza kunufaisha Watanzania. Lakini  tangu zimewezeshwa kifedha tayari matokeo yameanza kuonekana.
"Hii inafurahisha sana hizi taasisi zimewezsshwa na matokeo chanya tumeyaona, "alisema Manyanya.

Alisema kuwezeshwa kwa taasisi hizi pia kumesaidia  ukuaji wa viwanda nchini, na inatia moyo kuviwezesha zaidi..

Aidha amewahimiza Watanzania kuthamini vitu vinavyotengenezwa hapa nchini, ikiwamo kuthamini viwanda vidogo kwa sababu vinasaidia kutoa ajira kwa Watanzania, huku akiitaka SIDO kuhakikisha inasimamia wenye viwanda vidogo kuhakikisha wanapata mikopo kutoka benki ya kilimo Tanzania, TIDB, ili kuviongezea nguvu.

Alisema hakuna haja ya kubaki nyuma tunafanya kile tunachoweza na baadae kitaleta matokeo makubwa hapo baadae na kufikia Tanzania ya viwanda kama ilivyokusudiwa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais John P. Magufuli.

Alisema ni vema SIDO wakaweka jitihada ya kuwa karibu na watu hao ambao wakiwezeshwa wanaweza kuleta matokeo chanya katika kile ambacho wanafanya.

Mbali na hilo Naibu Waziri Manyanya amewapa wiki tatu TEMDO kuhakikisha wanawatengenezea mashine wajasiriamali ambao walitoa oda ya kutengenezewa mashine hiyo ili nao waendelee na shughuli ya uchakataji wa zabibu kwani mashine hizo ni nzuri na zina ufanisi wa hali ya juu.

Alisema hakuna sababu ya kuwacheleweshea kwa sababu wanahitaji kwa ajili ya kufanya maendeleo.

Kwa upande wake Meneja Taasisi ya ubunifu na uhandisi Mitambo, TEMDO, Mhandisi Alexander Komba, alisema kazi yao ni kubuni na kuendeleza Technolojia kwa ajili ya wajasiliamali wazalishaji, kisha kupeleka kwa SIDO ili ziweze kuwafikia walengwa. Kutokana na ushirikiano huo taasisi hizo mbili ambazo ziko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, waliweza kutatua changamoto ya kuchakata zao la Zabibu kwa haraka.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhandisi Stellah Manyanya, akizungumza na wakulima wakati wa uzinduzi wa  Technolojia mpya ya mashine ya kukamua mchuzi wa Zao la Zabibu katika kiwanda kidogo Cha WENDECE kilichopo Kata ya Hombolo Bwawani, Wilaya ya Dodoma.




 Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhandisi Stellah Manyanya,akikata utepe kuashiria uzinduzi wa  Technolojia mpya ya mashine ya kukamua mchuzi wa Zao la Zabibu katika kiwanda kidogo Cha WENDECE kilichopo Kata ya Hombolo Bwawani, Wilaya ya Dodoma.

Muonekano wa mashine ya kuchakata mchuzi wa Zabibu iliyobuniwa na kutengenezwa na TEMDO kwa ushirikiano wa SIDO.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhandisi Stellah Manyanya,akiangalia waini zinazotengenezwa  katika kiwanda kidogo Cha WENDECE kilichopo Kata ya Hombolo Bwawani, Wilaya ya Dodoma.





Prof. Kitila Mkumbo aanza kazi muda mchache mara baada ya kuapiswa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akimuapisha Profesa Kitila Alexander Mkumbo kuwa Waziri wa Viwanda n...