BRELA
YAKUTANA NA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA VIWANDA, BIASHARA NA MAZINGIRA NA KUTOA
TAARIFA YA MAJUKUMU YAO
Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imetoa elimu
ya Majukumu yao kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira
katika ukumbi wa Bunge leo tarehe 18/01/2020.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara
kwa kushirikiana na BRELA. Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa kuhusiana
na kazi na shughuli zinazofanywa na wakala katika kutoa huduma kwa jamii bila
kusahau changamoto mbalimbali zinazoikabili BRELA ili kamati iweze kushauri.
Katika mawasilisho yaliyotolewa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa
Brela Bi. Roy Mhando alieleza shughuli mbalimbali zinazofanywa na wakala ambazo
ni kusimamia Sheria ya Makampuni Sura ya 212, sheria ya majina ya biashara sura
ya 213, sheria ya alama za biashara na huduma, Sheria ya Usajili wa Hataza,
Sheria ya Leseni za Viwanda, Sheria ya Leseni za Biashara. Ameileza Kamati kuwa
Wakala inafanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha inatimiza majukumu yake kwa
ufasaha na kuwafikia wateja wake kwa kutoa elimu kwa njia mbalimbali ikiwemo
vyombo vya habari.
Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Kanali mstaafu Masoud
Ally Khamis (Mb) amempongeza Kaimu Afisa mtedaji Mkuu wa Wakala kwa kazi nzuri
anayoifanya na kuitaka Wakala kuendelea kutoa Elimu ili wadau wa biashara wajue
huduma mbalimbali wanazotoa hasa katika maeneo ya pembezoni ambapo wadau wa
biashara hawajui umuhimu wa kurasimisha biashara zao pia hawana uelewa wa
matumizi ya Tehama.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Lugha Bashungwa
(Mb) amewashukuru Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na
Mazingira kwa maoni na mawazo yao waliyoyatoa ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa
ya kuongeza ufanisi kiutendaji katika kuwahudumia wananchi pia ametoa maelekezo
kwa BRELA kuwa waweke mkakati wa mawasiliano wenye lengo la kutangaza huduma
zinazotolewa na Wakala kupita vyombo mbalimbali vya habari hasa kupitia redio
za kijamii.
Mbunge wa Sumve Mhe. Richard Ndasa ameipongeza BRELA katika
suala zima la kuwahudumia wateja kwani wamewawezesha wananchi wengi kupata
huduma kwa urahisi kwani hivyo ndivyo inavyotakiwa katika kufikia uchumi wa
kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025.
Mbunge wa Ndanda Mhe. Cecil Mwambe amewashauri BRELA wawemakini
kwenye kazi za kila siku ili kuondoa malalamiko na changamoto wanazopata wateja
hii itasaidia kuongeza idadi ya wateja na pato la Taifa kwa ujumla.
Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Hawa Mwaifunga ameiomba BRELA
wafike katika wilaya na Mikoa mbalimbali hapa nchi kwani huko kuna wadau wengi
wanaohitaji kujua faida za kurasimisha biashara zao.
Mbunge wa Monduri Julius Kalanga Laizer ameipongeza BRELA kwa
kuandaa mfumo wao ambao wanaendelea kuuhuisha na akapendekeza ni vema taasisi
zingine za biashara kuunganishwa pamoja.
Pia, amewapongeza watumishi wa BRELA kupitia kitengo cha
TEHAMA wanaotoa msaada kwa wateja katika matumizi ya mtandao wa BRELA kwani
wamekuwa wakisaidia sana wananchi pale wanapopata changamoto.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, Biashara na
Mazingira Mhe. Kanali mstaafu Masoud Ally Khamis (Mb) alihitimisha kikao kwa
kuwashukuru wajumbe wa kamati hiyo na kuwahimiza kuendelea kuishauri vema
Serikali ili kuweza kufikia adhima ya Uchumi wa Kati unaongozwa na Viwanda
ifikapo 2025.
![]() |
Waziri wa Viwanda na
Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) akizungumza wakati wa semina ya elimu
kwa wabunge wa kamati ya viwanda, biashara na mazingira.
|
![]() |
Mbunge Mhe. Hawa Mwaifunga (katikati) akizungumza wakati wa semina ya kamati ya Bunge Viwanda, Biashara na mazingira.
|


