Katibu Mkuu wizara ya viwanda na biashara Prof. Riziki Shemdoe ametoa wito kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini waje katika mkoa wa Tanga kwani yapo maeneo mengi ya kuwekeza katika sekta viwanda.
Wito
huo aliutoa jana alipotembelea kiwanda cha Nellkanth Chemical L.t.d kilichopo
eneo la Amboni jijini Tanga wakati alipofanya ziara ya siku moja.
Prof.
Shemdoe alisema kuwa Tanzania inavutia zaidi katika uwekezaji na maeneo
mengi ya uwekezaji yapo na yanatekelezwa kwa ajili yao hivyo kuwataka
wawekezaji wanaohitaji waje kuwekeza ili walipe kodi, walete ajira na mambo
mengine yanayoendana na uwekezaji.
“Wito
wangu kwa wawekezaji wengine waje wawekeze Tanzania, waje wawekeze mkoa wa
Tanga kuna maeneo mengi sana na magodauni ambayo yapo kwa sasa na yangeweza
kutumika kwa ajili ya viwanda, waje wakijua hapa nchini tuna blue print ambayo
inatekelezwa kwa ajili ya wawekezaji ili waje walipe kodi na kuleta ajira kwa
wananchi wetu” alisema.
Aidha
alizungumzia suala la uzalishaji katika kiwanda hicho na kusema kuwa kiwanda
hicho kina maeneo makubwa yanayofaa kuwekeza biashara zaidi ya uzalishaji
uliopo wa chokaa kwani wana maeneo mengine zaidi ya ekari 2,500 ambayo wanaweza
kulima chumvi ambayo imeshaanza kuonekana.
“Eneo
hili zamani lilikuwa halilimiki hapa lakini sasa kuna migodi ambayo inatoa
madini ambayo inazalishwa na kuleta faida nchini kwani wanalipakodi na kusaidia
wananchi kupata ajira, vilevile kuanzishwa kwa shamba hili kutatufanya sisi kuacha
kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi” alibainisha.
Hata
hivyo alisema kuwa kiwanda hicho kimefanya kazi kubwa kutokana na uzalishaji
wake kwani wameajiri wananchi zaidi ya 2,000 ambao wako kiwandani hapo na
wengine takribani 4,000 wako kwenye maeneo mengine ambayo yanamilikiwa na
mwekezaji huyo.
Naye
Mkurugenzi mzalendo wa kiwanda hicho Rashid Amour (Liemba) alisema kuwa kupitia
uzalishaji mkubwa wa kiwanda hicho tayari wameshateka masoko katika nchi
mbalimbali za Afrika mashariki na Maziwa makuu ambapo wamekuwa wakipeleka
bidhaa zao katika masoko ya ushindani.
“Kwakweli
mpaka sasa hivi soko letu kubwa liko Congo, lakini siyo Congo pekeyake bali
tumeziteka nchi za Kenya, Burundi, Rwanda na Uganda, kwa sasa hivi bidhaa yetu
tunashukuru tumezishika nchi zote za Afrika mashariki maana wao ndiyo
wanapambana na sisi” alifafanua Liemba.
“Kama
mnavyofahamu biashara ni ushindani na sisi tumeingia kwenye ushindani na nchi
hizi, tunaiomba serikali iweze kutusaidia katika ushindani huu na kama
itatusaidia nina hakika ushindani huu tutaushinda bila matatizo” aliongeza.
Aidha
alieleza kwamba kwa sasa ushindani mkubwa wanaoupata ni kutoka nchi ya Afrika
kusini ambako pia alizungumzia hofu yake kuhusu soko hilo kwamba nchi ya Congo
imeshaingiliwa na nchi ya China ambayo inatengeneza bidhaa hiyo ya chokaa
kupeleka huko.
“Kwa
sasa hivi ushindani wetu mkubwa uko South Africa kwa Congo, sasa hivi Congo
wameingia wachina, wachina wanajitahidi sana kutengeneza bidhaa kuleta hapa nao
ni chokaa kama sisi na mpaka sasa hivi tunajitahidi kupambana nao”
aliongeza.
Hata
hivyo alibainisha kwamba kiwanda hicho kinapambana katika soko la chokaa lakini
zipo biashara nyingine wanazozalisha kama vile magnissium (MGO) ambavyo vyote
vinatumika kusafishia cooper ambapo pia alitoa takwimu ya bidhaa
wanazosafirisha kupeleka kwenye masoko nje ya nchi.
“Congo
peke yake tunapeleka siyo chini ya tani elfu kumi lakini kipindi cha nyumba
tulikuwa tunakwenda mpaka tani elfu ishirini, Kenya na Zambia nako pia
tunapeleka tani kumi vilevile kwahiyo ni tani elfu ishirini kwa mwezi”
alifafanua.
![]() |
| Katibu Mkuu Prof. Riziki Shemdoe akipokea maelezo ya kiwanda cha Nellkanth Chemical L.t.d alipokitembelea kusikiliza changamoto za kiwanda hicho katika ziara yake ya kutembelea Viwanda Mkoani Tanga. |
