Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe, leo tarehe 20 Oktoba, 2020 ameiongoza menejimenti ya wizara katika kikao kazi cha kujadili mapitio (Background paper) ya sera ya viwanda vidogo na vya kati ya mwaka 2003.
Katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu ndugu Ludovick Nduhiye, wakuu wa Idara na Vitengo kutoka wizara ya viwanda na biashara, wawakilishi kutoka sekta binafsi (TPSF), Taasisi mbalimbali za serikali pamoja na wadau wa maendeleo nchini ambao ni Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT).
Prof. Shemdoe amesema
kwamba wizara imedhamiria kutunga sera za kuwawezesha wajasirimali wadogo
kuendeleza biashara ambapo katika blue print tozo mbalimbali ziliondolewa kwa
lengo la kuboresha mazingira bora ya wafanyabiashara. Hivyo katika sera hii
itawezesha wajasiliamali kufanya shughuli zao kwa urahisi pia uhakika wa mitaji
na mikopo.
Naye Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Kilimo cha Sokoine (SUA) Prof. Raphael Chibunda ameipongeza wizara kwa maamuzi
ya kuchagua eneo la SUA kwa ajili ya kikao kazi hicho pia amesema shughuli za
kilimo zinaenda sawia na uendelezaji wa viwanda ambayo ndio ajenda ya nchi hii, hivyo basi ili viwanda vizalishe bidhaa za kutosha ni lazima malighafi za kilimo ziwe za kutosha kukidhi viwanda vyetu, Prof. Chibunda alisema pia sera hiyo itasaidia wakulima wanaojishughulisha na uzalishaji wa mazao ya kilimo
kuwezeshwa katika mitaji na mikopo nafuu kuendeleza shughuli zao.
Mapitio ya sera ya viwanda vidogo na biashara ndogo yaliwasilishwa na mtaalamu mwelekezi ambaye ni Dkt. Josephat Kweka na kupokea maoni ya kuboresha maeneo mbalimbali kutoka kwa menejimenti ya wizara na wadau waliohudhuria kikao kazi hiki.
Katibu
Mkuu Prof. Riziki Shemdoe akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya wizara
mara baada ya ufunguzi wa kikao kazi cha mapitio ya sera ya Viwanda vidogo na
biashara ndogo katika ukumbi wa chuo cha SUA, MOROGORO.
Baadhi ya wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na wadau mbalimbali waliohudhuria kikao kazi cha mapitio ya sera ya Viwanda vidogo na biashara ndogo |