Search This Blog

Thursday, December 5, 2019

Mkutano wa Waziri wa Viwanda na Wadau wa sekta ya nyama na ngozi nchini

Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa Viwanda na Biashara akihutubia kwenye mkutano wake na wadau na wamiliki wa Viwanda vya nyama na ngozi nchini, kwenye ukumbi wa JNICC Jijini Dar es Salaam. 


Licha ya Tanzania kushika nafasi ya pili kwa wingi wa mifugo barani Afrika, lakini bado nchi hainufaiki na takwimu hizo kutokana na ubora mdogo wa mazao au bidhaa zitokanazo na mifugo.
Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa Viwanda na Biashara amebainisha hayo leo wakati alipokutana na kufanya kikao na wadau na wamiliki wa viwanda vya nyama na Ngozi nchini Tanzania kwenye Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
“Hadi sasa Tanzania ina ng’ombe zaidi ya milioni 32, mbuzi zaidi ya milioni 20 na kondoo zaidi ya milioni tano. Ili sekta hii iwe na tija kwenye uchumi wetu ni lazima uzalishaji wa bidhaa za ngozi na nyama unapaswa kuongezeka kwenye viwanda vyetu vya ndani” alibainisha kwenye hotuba yake ya ufunguzi.
Ili kukabiliana na hali hii, Mhe. Bashungwa alisema kuwa tayari ameshaanza mazungumzo na nchi ambazo zinaweza kutoa masoko makubwa ya bidhaa hizo, ambapo zitachangia kwa kiasi kikubwa uzalishaji kuongezeka na pia kuongeza pato la taifa. Ajenda ya Serikali ni kuhakikisha viwanda vinajengwa kwa wingi na kuweka mazingira sahihi ya kulinda bidhaa za viwandani na kuhakikisha viwanda hivyo vinazalisha ili hatimaye vilete faida kwa Tanzania na watu wake.
Kwenye mkutano huo, Mhe. Bashungwa aliweka bayana mikakati ya Serikali kulinda bidhaa hizo kama vile kutoza ushuru wa asilimia 80 ya thamani ya ngozi kuisafirisha nje ya nchi, lakini bado viwanda vya ngozi vinazalisha asilimia arobaini tu ya uwezo wa kuzalisha.  
Kwa upande wa wadau hao waliojitokeza kwa wingi, walisisitiza kuwa Serikali iendelee kuweka mazingira wezeshi na kuweka nia ya dhati na kufanya maamuzi ya kufanya biashara. Wazalishaji na wenye viwanda hawatafanikiwa iwapo Serikali haitaweka mkono wake, ikiwemo kutochelewesha maamuzi muhimu.
“Kwetu sisi wadau tunahitaji kuanza kuboresha mifugo yetu, kwasababu nyama nzuri yenye ubora, inatokana na ng’ombe bora. Hata kama Tanzania ina mifugo mingi lakini hatushindani kwenye soko kwasababu ng’ombe wetu sio bora kwenye export” alisema Mzee Crisant Mzindakaya ambaye anamiliki mifugo na kiwanda.
Majadiliano ya wadau na Serikali yametoa mwanga wa nini kifanyike ili sekta hiyo iwe na tija zaidi kwa taifa ikiwemo kuongeza uzalishaji wa viwanda hivyo. Kati ya viwanda vikubwa tisa vilivyopo nchini, viwanda vitano tu ndio vinavyofanya kazi ambapo vinazalisha chini ya asilimia arobaini ya uwezo wao wa kuzalisha.

MWISHO


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Viwanda na Biashara,
05 Desemba, 2019



Mhe. Bashungwa akiendesha mjadala kwenye kikao hicho ambapo wadau pamoja na Serikali waliweza kutoka na mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto zinazokinzana na ukuaji wa sekta hiyo muhimu nchini.



Pichani juu na chini, washiriki wa mkutano huo wakiwemo taasisi mbalimbali za Serikali kama vile Hazina, Brela, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Mambo ya Nje n.k. wakifuatilia mjadala wa mkutano huo.



Prof. Kitila Mkumbo aanza kazi muda mchache mara baada ya kuapiswa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akimuapisha Profesa Kitila Alexander Mkumbo kuwa Waziri wa Viwanda n...